
Tukio
hilo limeelezwa kufanyika katika eneo la Bahari ya Hindi "ukishapita
Msasani" ambako kuna mkondo wa maji unaodhaniwa kusababishwa na kina
kirefu cha maji.
Eneo
hilo lipo mwendo wa nusu saa kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kwa boti
ziendazo kasi. Safari mpaka Zanzibar huchukua saa mbili.
Video
hiyo inaonyesha abiria hao wakiwa wanashangaa uamuzi wa mtu huyo
kujitosa baharini huku wengine wakisikika wakisema kuwa anaonekana
akiogelea.
Baadhi
ya waliokuwa kwenye boti hiyo walisikika kwenye video hiyo wakiomba
wapewe nafasi wajitose kwenda kumtafuta kwani wao ni mahiri kwenye
uogeleaji.
"Kama
vipi tumfuate, wengine tunaweza (kuogelea)... anaonekana yule, kuleee
tuacheni sisi tunaoweza kuogelea tukamchukue kwasababu tunaweza jamani,"
alisikika mtu huyo akimwomba mmoja wa wahudumu wa boti hiyo huku
akirekodi video.
Taarifa
kutoka ndani ya Azam zilisema mabaharia wa boti hiyo walijitahidi
kumtafuta mwanaume huyo eneo alipojitosa lakini hawakufanikiwa.
"Baada
ya mwanaume huyo kujirusha baharini nahodha wa boti aliambiwa na
aliirudisha boti nyuma hadi eneo linalodhaniwa kuwa ndipo alipojitosa,
lakini hawakufanikiwa (kumuona). Walirudi wenyewe tu," alisema mmoja wa
mashuhuda.
Aidha,
shuhuda huyo alisema baada ya kumkosa, walijadiliana kwa muda kuhusu
nini kinaweza kufanyika na hatimaye waliona hawana namna zaidi ya
kuendelea na safari ya Zanzibar.
Alipoulizwa
kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jumanne
Murilo alisema waulizwe watu wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Alipotafutwa
kuzungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Lazaro Mambosasa alisema ofisi yake bado haijapewa taarifa
yoyote kuhusu mkasa huo.
"Sasa
kama amejitosa baharini wanasema amekufa au wamefanikiwa kumwokoa?"
Aliuliza Kamanda Mambosasa. "Mimi hizo taarifa ndiyo kwanza nazisikia
kutoka kwako."
Aprili
5, mwaka jana msichana mmoja mwenye umri wa miaka 16 aliyekuwa
mwanafunzi wa kidato cha tatu katika sekondari moja ya Zanzibar,
alijitosa baharini katika eneo la Chumbe.
Msichana
huyo alijirusha kutoka katika boti ya Azam ya Kilimanjaro V akisafiri
na mjomba wake kutoka jijini kuelekea Unguja, lakini aliokolewa na
mabaharia wa chombo hicho.
Baadaye
wanafamilia wa msichana huyo waishio Kikwajuni, Unguja walisema chanzo
cha msichana huyo kutaka kujiua ni kukutwa na simu ambayo alishindwa
kueleza alikoipata na kukimbilia Dar es Salaam kabla ya kufuatwa.